Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, ifuatayo ni matini ya taarifa ya Ayatullah A'rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini Irani, inayolaani kutolewa hukumu za dhuluma na ukatili na mahakama za eneo hilo dhidi ya wananchi, vijana na maulamaa wakubwa, hususan hukumu isiyo ya haki iliyotolewa na watawala wa Kuwait ya kunyongwa mwanazuoni mpambanaji asiyekata tamaa, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Hussein al-Matouq:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
«مِنْ أَجْلِ ذَٰلِکَ کَتَبْنَا عَلَیٰ بَنِیٓ إِسْرَآئِیلَ أَنَّهُ مَنْ قَتَلَ نَفْسًا بِغَیْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِی الْأَرْضِ فَکَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِیعًا وَمَنْ أَحْیَاهَا فَکَأَنَّمَآ أَحْیَا النَّاسَ جَمِیعًا ۚ وَلَقَدْ جَآءَتْهُمْ رُسُلُنَا بِالْبَیِّنَاتِ ثُمَّ إِنَّ کَثِیرًا مِنْهُمْ بَعْدَ ذَٰلِکَ فِی الْأَرْضِ لَمُسْرِفُونَ»
«Kwa sababu hiyo, tuliwaandikia Wana wa Israili kwamba: Yeyote atakayemuua mtu bila ya mtu huyo kuua au kufanya ufisadi katika ardhi, basi ni kana kwamba amewaua watu wote. Na yeyote atakayemuokoa mtu, basi ni kana kwamba amewaokoa watu wote. Na hakika Mitume Wetu waliwajia na hoja zilizo wazi, lakini baada ya hayo, wengi wao wakawa ni wenye kupita kiasi katika ardhi.»
(Suratul-Ma'idah: 32).
Wakati ambapo ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na changamoto zisizo na mfano wa awali kutokana na njama pana na zilizopangwa kwa utaratibu na maadui wa Uislamu, hususan utawala wa Marekani wenye kiburi cha kujiona mkuu na utawala wa Kizayuni, kusikia habari za hukumu za dhuluma na ukatili zinazotolewa na mahakama za eneo hilo dhidi ya wananchi, vijana na maulamaa wakubwa, hususan hukumu isiyo ya haki ya watawala wa Kuwait ya kunyongwa mwanazuoni mpambanaji asiyekata tamaa, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Haj Sheikh Hussein al-Matouq, mwanazuoni mkubwa na mtumishi wa wananchi wa Kuwait, kumeumiza nyoyo za Waislamu na kuibua wimbi la ghadhabu na huzuni miongoni mwa Umma wa Kiislamu, pamoja na vituo vya kielimu na Hawza za kielimu nchini Iran na duniani kote.
Hatua hii, ambayo imechukuliwa kwa kupuuza waziwazi misingi ya kisheria, kibinadamu na nafasi tukufu ya maulamaa wa dini, imevuka mipaka ya hukumu ya mahakama pekee. Bali, ni aina ya shambulio dhidi ya utambulisho na haki za kidini za Waislamu na Waislamu wa madhehebu ya Shia, na ni jaribio la wazi la kudhoofisha ushawishi na heshima ya maulamaa wa Kiislamu.
Mimi, kwa kutegemea aya hii tukufu ya Mwenyezi Mungu:
«أَنَّهُ مَنْ قَتَلَ نَفْسًا بِغَیْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِی الْأَرْضِ فَکَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِیعًا...»
«Yeyote atakayemuua mtu bila ya mtu huyo kuua au kufanya ufisadi katika ardhi, basi ni kana kwamba amewaua watu wote...»
Na kwa kukumbusha ukweli huu kwamba kumdhulumu Muumini ni dhambi isiyosameheka, ilhali Waumini wote ni ndugu wanaosimama pamoja chini ya bendera ya umoja na katika kivuli cha neno la Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Mtukufu, na kwamba heshima na utukufu wao ni lazima vilindwe; kwa niaba ya Hawza za kielimu, Maraji' wakubwa wa Taqalidi, walimu waheshimiwa na taasisi zinazohusiana nazo, huku nikilaani mwenendo huu wa dhuluma na hukumu iliyotolewa kinyume cha sheria, nasisitiza kwamba, ni wajibu wa serikali na mamlaka zinazohusika nchini Kuwait, kwa kuzingatia msingi wa udugu wa Kiislamu, kufanya mapitio ya haraka ya hukumu hii, kwa kuzingatia haki za msingi za taifa tukufu la Kiislamu, hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Kuwait, pamoja na kuheshimu nafasi ya kielimu na kidini ya watu mashuhuri; ili kuzuia kutokea kwa janga hili na kukwepa haki.
Jambo jingine muhimu linalopaswa kuzingatiwa ni kwamba aina yoyote ya ubaguzi katika kuwachukulia maulamaa wakubwa na viongozi wa kidini halileti tu ukiukwaji wa haki za mtu binafsi na za kijamii, bali inaweza pia kuandaa mazingira ya kuibuka mifarakano na tofauti baina ya nchi za Kiislamu, hili ndilo hasa jambo ambalo maadui wa Uislamu wanalolitarajia, na ni lazima serikali na mataifa yote ya Kiislamu waliepuke.
Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azijaalie serikali za Kiislamu kupata mwamko na utambuzi, na aujaalie Umma wa Kiislamu kupata ushindi dhidi ya maadui wa Kimarekani na Kizayuni.
Alireza A'rafi
Mkurugenzi wa Hawza Nchini Iran
Maoni yako